Jumapili 19 Oktoba 2025 - 00:23
Rais wa Colombia atenga dhahabu iliyokamatwa ili kuwsaidia watoto waliojeruhiwa Ghaza

Hawza/ Rais wa Colombia, Gustavo Petro, ametoa agizo kwamba dhahabu ya magendi iliyokamatwa ikihusishwa na “Jumuiya ya Mali Maalumu” itumike kutoa misaada ya kitabibu na kusaidia ujenzi upya wa miundombinu iliyoharibiwa huko Ghaza.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Petro aliandika katika akaunti yake rasmi kwenye mtandao wa kijamii X akisema:

“Nimeiagiza Jumuiya ya Mali Maalumu kutumia dhahabu iliyokamatwa kwa ajili ya matibabu ya watoto waliojeruhiwa huko Ghaza.”

Alisisitiza kwamba, lengo la hatua hii linazidi misaada ya dharura, na kwamba anapanga kuwasilisha rasimu ya azimio katika Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuanzisha “jeshi la kimataifa” litakaloshiriki katika ujenzi upya wa Ghaza na kuliunga mkono taifa la Palestina.

Tangia mwanzo wa mgogoro wa Ghaza, Petro amekuwa akichukua msimamo wa wazi na wa kimapambano, na hapo awali alilaani kukamatwa kwa raia wawili wa Colombia katika operesheni ya “Sumud Humanitarian Fleet” iliyotekelezwa na wanajeshi wa Israel.

Alilitaja tukio hilo kuwa “uhalifu wa kimataifa”, na akatangaza kuwa serikali ya Colombia, kupitia njia za kidiplomasia na za ubalozi, imehakikisha haki za raia hao zinalindwa, na kwamba baadhi yao wamerudishwa Colombia kwa msaada wa “Mfuko Maalumu wa Uhamiaji.”

Petro alibainisha kwamba rasilimali zinazotumwa Ghaza hazitoki kwenye bajeti ya umma, bali zinatokana na mali zilizokamatwa katika kesi za jinai dhidi ya mashirika ya kihalifu. Alisema hatua hiyo ni sehemu ya sera ya mambo ya nje yenye kuzingatia utu ya serikali yake, akiongeza:

“Colombia inaweza kuchukua jukumu muhimu katika kuijenga upya Ghaza na kuwasaidia watoto na familia zilizoathirika.”

Uamuzi huu ni alama ya mshikamano kati ya Colombia na taifa la Palestina, na ni jitihada za kufidia uharibifu ulioletwa na vita na ukosefu wa usawa wa kibinadamu. Pia unaonesha kwamba serikali ya Petro, mbali na msimamo wa kisiasa, inaweka mkazo katika vitendo vya kupunguza mateso ya kibinadamu.

Wataalamu wa haki za binadamu wametaja hatua hiyo kuwa hatua chanya katika kuwasaidia watoto na raia wasiokuwa na hatia walioko katika maeneo yenye migogoro ya kibinadamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha